HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA

 

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA, VIWANJA VYA KARIMJEE, DAR ES SALAAM, TAREHE 24 OKTOBA 2018

 

SALAMU

Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

Bw. Alvaro Rodriguez, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP);

Mheshimiwa Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih, Balozi wa Comoro na Kiongozi wa Mabalozi nchini;

Mheshimiwa Charles Mwita, Msahiki Meya wa Jiji la Dar-es-Salaam;

Waheshimiwa Mabalozi;

 

Waheshimiwa Mabalozi wote na Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umoja wa Mataifa nchini mliopo hapa;

Makatibu Wakuu waliopo hapa;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

 

Habari za Asubuhi..!!

 

UTANGULIZI

Ninayo furaha kubwa kujumuika nanyi leo hii katika kuadhimisha miaka 73 ya Umoja wa Mataifa. Siku hii ni ya kipekee hasa kwa kuzingatia majukumu makubwa yanayotekelezwa na Umoja wa Mataifa katika kuifanya dunia kuwa ya amani, salama kwa kila mmoja kuishi na yenye maendeleo endelevu kwa wote.

Aidha, napenda kuwafikishia salamu kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia kwako, Mratibu Mkaazi, Mheshimiwa Rais anatoa pongezi zake kwa Bwana António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa Jumuiya za Umoja wa Mataifa kwa ujumla wakati tukiadhimisha miaka 73 ya Umoja wa Mataifa.

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Waheshimiwa Mabalozi;

na Watanzania wenzangu mliopo hapa,

Tarehe 18 Agosti 2018, dunia ilipokea kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Hayati Kofi Annan.  Natumia nafasi hii kwa mara nyingine kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kwa ujumla,kufuatia kifo hicho.

Kwetu sisi Hayati Kofi Annan atabakia kuwa mfano mzuri kwa  uhodari  wake katika kuifanya dunia kuwa sehemu salama yenye amani, maendeleo, na utawala wa sheria. Ni jukumu letu sisi tuliobaki kuendeleza mazuri aliyoyafanya.  Mungu ampe pumziko la milele. Amina!

Nitumie nafasi hii pia, kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa salamu za pole na msaada wa hali na mali kufuatia maafa yaliyosababishwa na ajali ya kivuko cha  MV Nyerere, iliyotokea tarehe  20 Septemba, mwaka huu katika Ziwa Vicktoria ambapo Watanzania zaidi ya 217 walipoteza  maisha. Kufuatia tukio hilo, Serikali ilifungua akaunti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ajali hiyo na Umoja wa Mataifa umeshiriki kwa kutoa salamu za pole na kuwatakia pole ndugu zetu waliopotelewa na ndugu zao. Fedha hizo na misaada mbalimbali iliyotumwa kwetu tunawahakikishia kwanba zitatumika kuwasaidia waathirika na familia zao, pamoja na kuchangia ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya Wilaya kwa wakazi wa maeneo husika. 

Aidha, Serikali imeunda Tume maalumu ili kuchunguza tukio la ajali hiyo na kubaini chanzo chake. Lengo la kufanya hivyo, ni kusaidia upatikanaji wa taarifa muhimu ili Serikali iweze kuchukua hatua muhimu katika kudhibiti maafa namna hiyo kutojirudia tena kwenye maeneo yetu yanayotumia vyombo vya majini. Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

Naomba wote tusimame kwa dakika moja kumkumbuka Hayati Kofi Annan na Watanzania wenzetu waliopoteza maisha kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

KAULIMBIU YA MAADHIMISHO

Waheshimiwa mabalozi, Ndugu Watanzania na Wageni Waalikwa,

Kaulimbiu ya Maadhimisho haya Uwezeshaji wa Vijana na Ubunifu katika Kufikia Malengo ya Maendelo Endelevu (Youth Empowerment and Innovation for achievement of the Sustainable Development Goals) imebeba dhana kubwa kwa Taifa na dunia kwa ujumla. Kaulimbiu hii inatoa kipaumbele kwa vijana ambao ndio nguvu kazi na wadau muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu yanayolenga kutomuacha yeyote nyuma.

Katika kuonesha msisitizo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezindua Mkakati wa Vijana wa Umoja wa Mataifa ujulikanao kama “United Nations Youth Strategy”, tarehe 24 Septemba, 2018. Mkakati huo umekuja kipindi muafaka ambapo tunashuhudia dunia ikiwa na vijana takribani bilioni 1.8 wenye umri kati ya miaka 10 na 24, idadi hii ni kubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Na hapa nchini tuna idadi kubwa ya vijana na kama ambavyo mwakilishi wa vijana alivyosema upo umuhimu wa kuona namna nzuri ya kuweka mikakati kwa ajili ya vijana wetu.

Mkakati huu umekuja kipindi ambacho vijana wanakumbwa na changamoto za utandawazi, teknolojia, umaskini, ukosefu wa ajira, matumizi ya dawa za kulevya, mabadiliko ya tabianchi, na changamoto nyingine nyingi. Hivyo, pasipo kuwa na mikakati ya makusudi ya kukabiliana na changamoto hizi, dunia itapoteza mwelekeo na nguvu kazi kubwa. Kwa hali hiyo, itakuwa vigumu sana kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Wageni Waalikwa,

Kwa upande wa Tanzania, vijana ni hazina kubwa kwa kizazi cha sasa na cha baadaye. Tanzania ina idadi ya vijana zaidi ya milioni kumi na tano (15,587,621) ambayo ni sawa na asilimia 34.7 ya idadi ya Watanzania wote. Idadi kubwa ya vijana na uwezo wao wa kuelewa haraka unawafanya wawe sehemu muhimu katika kuchangia kukua kwa uchumi.  Kwa hiyo, vijana wakiandaliwa ipasavyo, watakuwa ni chachu kubwa ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Serikali imeweka mkakati maalum kwa vijana ikiwemo kuanzisha Kurugenzi na Wizara Maalum inayoshughulikia vijana.

Kwa kutambua umuhimu wa vijana, Tanzania imeweka mikakati mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Elimu ambayo imelenga kuhakikisha vijana wanapata elimu sambamba na kuwajengea ujuzi katika taaluma mbalimbali.

Katika kufanikisha azma hii, Serikali inatoa elimu bure kuanzia shule za awali mpaka sekondari pamoja na kuanzisha vyuo vya ufundi katika Mikoa yote ya Tanzania. Kwa mfano, hadi sasa kuna vyuo vya ufundi takribani 672 nchini.

Vilevile, Serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu. Katika mwaka wa masomo 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 427.55 zimetumika kama mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Jumla ya wanafunzi 122,623 (mwaka wa Kwanza 33,857 na wanaoendelea 86,766) wamenufaika na mikopo hiyo.

 

AJIRA KWA VIJANA

Wageni Waalikwa,

Katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana, Tanzania ilianzisha Sera ya Ajira ya Taifa ya mwaka 1997. Sera hii iliboreshwa zaidi mwaka 2008 ili iendane na mabadiliko ya soko la ajira na uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki pamoja na changamoto za ajira zinazotokana na utandawazi.

Vilevile, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021, unalenga kuifanya Nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Mpango huu unalenga kupunguza ukosefu wa ajira nchini kwa njia ya viwanda na kukuza upatikanaji wa viwanda vinavyohitaji  uzalizashaji wa bidhaa zingine pamoja  na utoaji wa huduma.

Katika kutekeleza mpango huu, mikakati mbalimbali imeanzishwa kama njia za kukuza ajira kwa vijana. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na: Uanzishwaji wa Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) kwa lengo la  kuwapa vijana miongozo itakayowasaidia kupata ajira zinazoendana na taaluma zao; Kuingiza miongozo ya ajira na kazi za Umoja wa Mataifa (United Nations Chief Executive Board (UN-CEB)katika sera za ajira na mipango ya maendeleo ya Nchi na Uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Jamii  kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Pia, katika kuhakikisha vijana wanajifunza kazi na kupata ujuzi zaidi, mwaka 2017, Serikali ilianzisha mpango wa Kitaifa wa kuhakikisha vijana wanapata nafasi za mafunzo ya kazi. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2016/2017 zaidi ya vijana 11,500 walifaidika na mpango huo.

Aidha,  Serikali ya Awamu ya Tano inafanya jitihada kubwa kuvutia wawekezaji kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Aidha, Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa  kwenye ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme, ujenzi wa barabara, upanuzi wa bandari, na ujenzi wa miundombinu ya nishati.

Utekelezaji wa miradi hii ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana nchini na pindi itakapokamilika itaendelea kuwawezesha vijana wengi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa gharama nafuu na tija. Napenda kutoa rai kwa vijana wote nchini kutochagua kazi na badala yake wachangamkie fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi hii mikubwa.

Pamoja na jitihada hizi nyingi za Serikali katika kuwawezesha vijana bado kuna changamoto. Hivyo, tunauomba Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wote wa maendeleo kuunga mkono jitihada hizi za Serikali kwa kuwapa vijana wetu fursa za kazi, mafunzo ya kazi “Internships” na fursa za kufanya kazi kwa kujitolea hasa kupitia Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kujitolea yaani “United Nations Volunteering”.

Tunawashukuru wadau wa maendeleo kwa kutoa nafasi za masomo “scholarships” kwa vijana wa Kitanzania. Tunaomba nafasi hizo ziendelee kutolewa hususan katika fani za madini, nishati na masomo ya sayansi kwa ujumla.

 

UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Pamoja na kuongelea kaulimbiu ya maadhimisho haya, napenda pia kutumia nafasi hii kuongelea japo kwa uchache masuala mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa kwa pamoja na Serikali tunaendelea kushirikiana vizuri katika kutekeleza masuala yayayogusa maendeleo na huduma kwa jamii kama vile Elimu, Afya Maji pamoja na maeneo mengine ya maendeleo. Jambo hili kwa niaba ya Serikali pamoja na Watanzania wote napenda kutoa shukurani zangu kwenu viongozi wote wa Umoja wa Mataifa kwa jitihada kubwa mnazozifanya za kuunga mkono Jitihada za Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.

Tanzania katika kutekeleza Kama mnavyofahamu,Serikali imeendelea kutekeleza kwa kasi, Malengo ya Maendeleo Endelevu. Utekelezaji wa Malengo hayo nchini ulianza rasmi tangu mwaka 2016 kwa kuingizwa kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya Nchi ili kuendana na vipaumbele vyetu hasa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021) na Mkakati wa Kukuza uchumi na Kupunguza Umaskini, Zanzibar (MKUZA III).

Kwa lengo la kujitathmini na kuboresha mikakati ya utekelezaji wa Malengo hayo, Serikali imejiandikisha kufanya mapitio ya hiari ya Nchi ya utekelezaji wake (Voluntary National Review – VNR) katika Mkutano wa Jukwaa la Kisiasa la Ngazi za Juu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (High Level Political Forum (HLPF) utakaofanyika New York, Marekani mwezi Julai mwaka, 2019.

Tayari, Kikosi Kazi maalum kimeundwa kwa ajili ya kuandaa taarifa hiyo kwa ufanisi. Serikali inajiandaa kufanya mapitio ya malengo yafuatayo: Lengo Namba 4 “elimu bora”; Lengo Namba 8 “kazi nzuri na ukuaji wa uchumi”; Lengo Namba 10 “kupunguza hali ya kutokuwepo usawa”; Lengo Namba 13 “kuchukua hatua kuhusu hali ya Nchi” na Lengo Namba 16 “amani, haki na taasisi imara”. 

HAKI ZA BINADAMU

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Kukuza, kuimarisha na kulinda Haki za Binadamu ni wajibu wa msingi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuzingatia umuhimu wa haki za binadamu kwa watu wake, mwaka 1984, Serikali ya Tanzania iliingiza Sheria ya Haki za Binadamu katika Katiba ya Nchi ambayo inatoa haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa wananchi, kwa kufuata kanuni za haki za binadamu zilizoainishwa katika Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, lililopitishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948.

Vilevile, Serikali imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za kiraia na ule wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni.Sambamba na kusimamia haki hizo, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama, kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na Katiba na Sheria za Nchi. Sheria za Nchi zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari. Hakuna ubanaji wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali. Hili linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152 ambapo kati ya hivyo, vitatu vinamilikiwa na Serikali. Mwananchi yeyote akienda kinyume na sheria, Serikali inawajibika kwa mujibu wa Sheria na Taratibu za Nchi. 

 

KUHUDUMIA WAKIMBIZI

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuwapokea na kuwahifadhi watu wote wanaokimbilia nchini kutokana na migogoro, vita na ukosefu wa amani na kuhofia usalama wa maisha yao katika Nchi zao. Tangu tupate Uhuru chini ya Rais wa Kwanza Mwalimu J.K. Nyerere, msimamo wa Nchi yetu umekuwa kujali na kuhifadhi utu, hadhi, haki, na usalama wa maisha ya binadamu wote.

Msingi huu, umeifanya Nchi yetu kuwa kimbilio la watu wa Nchi nyingine wanaopata matatizo katika Nchi zao. Tanzania imeridhia pia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu watu wanaolazimika kuzikimbia Nchi zao kwa kuhofia maisha yao ambapo imekuwa ikiwajibika kuwapokea wakimbizi na kuwahifadhi nchini.

Pamoja na kuridhia mikataba hii ya Kimataifa, shughuli za wakimbizi nchini zinaongozwa na Sheria ya Wakimbizi Namba 9 ya mwaka 1998 na Sera ya Taifa ya Wakimbizi ya mwaka 2003. Katika Sera na Sheria zetu imesisitizwa kuwa Nchi yetu itawahifadhi wakimbizi kwa kipindi ambacho Nchi zao zina matatizo ya usalama na amani na hawawezi kurejea; pale hali ya amani na usalama inapoimarika, Wakimbizi hao wanapaswa kurejea makwao.

Tangu mwezi Septemba mwaka jana, Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) imekuwa ikiwarejesha kwa hiari wakimbizi kutoka Burundi katika Nchi yao. Zoezi hili limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa wakimbizi hao.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni Serikali imekuwa ikipokea shutuma kutoka kwa baadhi ya Jamii ya kimataifa kuhusu uendeshaji wa zoezi hilo.  Napenda kusisitiza kuwa zoezi hili ni la hiari na Serikali imelitekeleza baada ya kujiridhisha kuwa hali ya amani na usalama imerejea nchini Burundi. Hivyo, hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao wameamua kurejea nchini kwao ili kuendelea na shughuli za kulijenga Taifa lao.  

Hadi sasa tayari wakimbizi 52,283 wa Burundi wamerejea nchini kwao kati ya wakimbizi 81,281 waliokwisha jiandikisha. Tunatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na washirika wengine wa Mandeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili kufanikisha zoezi la kuwarejesha wakimbizi kwa hiari na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

HITIMISHO

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Naomba nimalizie kwa kusisitiza tena kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na taasisi zilizopo chini yake itaendelea kushirikiana na Taasisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa nchini katika kuhakikisha Mkakati wa Vijana wa Umoja wa Mataifa unakuwa ni dira ya kuwafanya vijana wetu kuwa chachu ya maendeleo duniani kote.

Napenda kutumia nafasi hii kupongeza Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo hapa nchini kwa kuunga mkono Mkakati wa Serikali wa kuhamisha Makao Makuu kwenda Dodoma ambako Umoja wa Mataifa tayari wameshahamia.

Mwisho, ni matumaini yangu kwamba kufuatia Serikali kuhamia rasmi makao makuu ya Nchi jijini Dodoma, maadhimisho ya mwaka 2019, nayo yatafanyika katika Jiji la Dodoma. Kufanyika kwa maadhimisho yajayo jijini Dodoma, kutatoa fursa pia kwa wananchi na wakazi wa Jiji hilo kushuhudia upandishaji wa bendera ya Umoja wa Mataifa.

Naomba niwatakie wote mliopo hapa na watu wote duniani Siku ya Furaha ya Kuzaliwa kwa Umoja wa Mataifa na kwa Kutimiza miaka Sabini na Tatu!!!.

                              Ahsanteni sana!