Press Releases

Bosi wa UN apongeza juhudi za pamoja katika maendeleo mkoani Mtwara

TAARIFA YA HABARI YA PAMOJA

Imezuiwa hadi Juni 29, saa 9 Alasiri

Bosi wa UN apongeza juhudi za pamoja katika maendeleo mkoani Mtwara  

 

Maofisa wa UN, Serikali na Jukwaa la Wahariri Tanzania washuhudia wenyewe juhudi zinazofanywa

29 Juni, Mtwara – Umoja wa Mataifa (UN) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo wameendesha warsha ya pamoja kwa waandishi wa habari 30 kutoka mikoa ya Ruvuma, Pwani, Mtwara na Lindi. Warsha hiyo ililenga kuwajengea waandishi uelewa kuhusu miradi inayotekelezwa na UN katika mikoa yao na kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuandika habari za maendeleo katika muktadha wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Warsha hiyo ilitanguliwa na ziara katika miradi miwili ya UN mkoani Mtwara iliyotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, ujumbe huo ulizuru programu inayofadhiliwa na UNICEF, ambayo inahusisha ushirikiano na serikali na sekta binafsi, katika kufanya mchakato wa kufanya usajili wa vizazi kuwa rahisi. Mradi huo unatumia njia ya ujumbe mfupi wa simu.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari, Mratibu Mkazi wa UN, Bw. Alvaro Rodriguez, alipongeza utaratibu wa kushirikiana katika kutekeleza programu mikoani na alitoa wito kwa waandishi wa habari kuandika habari za shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na UN, serikali na washirika wengine kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Dunia. “Mradi wa UNICEF wa usajili wa vizazi na miradi mingine inayotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama vile UNESCO ambayo inashirikiana na vituo vya redio za jamii mkoani hapa inaonyesha mchango chanya ambao UN, serikali na washirika wengine wanatoa katika mikoa yote nchini Tanzania tunapoendelea na utekelezaji wa Malengo ya Dunia,” alisema Bw.  Rodriguez. “Kwa kushirikiana kwa karibu na TEF, tunatarajia kuwajengeeni ninyi uwezo ili mwangazie hatua hizi ambazo zinaleta tija na hivyo kuyapa maeneo yaliyo pembezoni sauti na hasa kwa wale ambao bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali,” aliwaeleza waandishi wa habari kutoka katika mikoa minne.

Kwa mujibu wa UNICEF, mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano unaofanyika katika ngazi ya mikoa ulizinduliwa kwa msaada wa UNICEF katika mikoa ya Mtwara na Lindi mwezi Septemba, 2017, na tangu hapo mfumo huo mpya umekuwa ukiendelea katika vituo vyote vya afya na ofisi za kata kote katika halmashauri za wilaya kwenye mikoa hiyo miwili. Kwa kuwaruhusu akina mama, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya mbali, kusajili uzazi wa watoto wao kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, programu hiyo inawarahisishia watumishi wa afya kupokea taarifa na kuandaa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa na TEF walishuhudia kwa kusikia wenyewe kutoka kwa maofisa wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), watumishi wa afya na akina mama jinsi programu hiyo inavyorahisisha kazi yao na kuongeza idadi vya vizazi vinavyosajiliwa.

Licha ya programu ya UNICEF, ile ya UNESCO mkoani Mtwara inatoa msaada kwa vituo vya redio za jamii kuandaa vipindi vinavyohamasisha uraia mwema na utaratibu wa ujumuishi. Mfano ni pamoja na vipindi vinavyotoa mafunzo kuhusu madhara ya vitendo vya ukeketaji (FGM) na ubaguzi dhidi ya makundi ya watu walio hatarini kama vile wale wenye ualbino. Vilevile, UNESCO inahamasisha matumizi ya redio za jamii kuandaa vipindi vya uwezeshaji wanawake na vijana katika maeneo ya mbali yasiyofikika kwa urahisi kwa kuwapa taarifa wanazoweza kutumia.

 

Maelezo kwa Wahariri:

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Umoja wa Mataifa Tanzania, kupitia Kundi Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (UNCG), zimeshirikiana kwa zaidi ya miaka 5 na ushirikiano huu wa sasa hivi unaendeleza ushirika huu kwa kuimarisha idadi ya shughuli ambazo zitaendeshwa kwa pamoja na pande mbili. Ujumbe wa UN na TEF wametoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Pwani, Lindi na Mtwara kuhusu uandikaji taarifa za maendeleo na UN na utekelezaji unaofanywa na serikali wa Malengo ya Dunia. Mafunzo ni ya pili katika kanda tano za mafunzo kwa vyombo vya habari ambayo yatatolewa kote nchini, ambapo ya kwanza yalifanyika mwezi uliopita mkoani Kigoma.

Kuna zaidi ya miradi 20 inayotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa katika mikoa ya kusini.