Press Releases

UN & SEED Trust Zaungana ili Kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Imezuiwa hadi MCHANA wa tarehe Mei 18

 

UN & SEED Trust Zaungana ili Kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu

 

Watu wenye ulemavu wajumuishwa kwenye Kampeni ya Malengo ya Dunia

 

18 Mei 2018, Dar es Salaam – Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, Umoja wa Mataifa umewapa mafunzo na kuwatunuku vyeti watu wenye ulemavu ili watekeleze wajibu wao katika kufikiwa kwa Malengo ya Dunia. Mpango huu unatekelezwa kwa kushirikiana na SEED Trust – hii ni AZISE inayolenga kuwajengea uwezo wa kijamii na kiuchumi Watanzania wenye ulemavu. Watu 25 wenye ulemavu walitunukiwa vyeti kuwa Mabingwa wa Malengo ya Dunia, hii inafanya idadi ya mabingwa waliopata mafunzo hayo kufikia 1,500. Mafunzo hayo yanawapa mamlaka ya kuwa mabalozi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hasa katika kutoa elimu na kuwa sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Dunia katika jamii zao kwa kuweka mkazo maalumu katika kuwafikia watu wengine wenye ulemavu. Utoaji wa vyeti kwa watu hawa 25 wenye ulemavu ni sehemu ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kutomwacha yeyote nyuma kama inavyosisitizwa katika Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Mabalozi hawa wapya wa Malengo ya Dunia wataendesha kampeni na kutetea upatikanaji wa suluhu kwa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Watawekea mkazo masuala yanayohusiana na watu wenye ulemavu kwa malengo manne kati ya 17 ya dunia ambayo ni Lengo la 3: Afya njema na ustawi, Lengo la 4: Elimu Bora, Lengo la 5: usawa wa jinsia, Lengo la 8: Kazi zenye Staha na Ukuaji wa Uchumi na Lengo la 10: Kupunguza utofauti wa kimapato.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez, Bi. Hoyce Temu, Mtaalamu wa Mawasiliano wa UN, alisema, “Malengo ya Dunia ni ya wote na ni jumuishi—kila mmoja anaitwa kushiriki na hii ni pamoja na watu wenye ulemavu ambo ni miongoni mwa watu wanaobaguliwa sana. Sisi kutoka UN tunataka watu wenye ulemavu kuyaelewa Malengo ya Dunia na kutekeleza sehemu yao.” Aliongeza kwamba, “Kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali na SEED Trust, tunataka hawa Mabingwa wapya wa Malengo ya Dunia kuonyesha kwamba hali ya kuwa na ulemavu kusizuie kutimiza wajibu wako katika maendeleo ya Tanzania.”

Akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu na kuendeleza ushirikiano wao na Umoja wa Mataifa katika shughuli za maendeleo, Bi. Margaret Mkanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Seed Trust Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu akiwakilisha wenye ulemavu alisema, “Watu wenye ulemavu walikuwa muhimu sana katika kuandaa mpango huu wa kimaguezi kuelekea katika baadae iliyo bora, sasa ile kazi yenyewe ya kuleta mabadiliko yanayotakiwa iko hapo mbele tu. Watu wenye ulemavu ni lazima waongoze; watoe mwongozo kwa dunia katika kufikia malengo haya kwa ajili ya kila mmoja. Safari hii inahitaji ustahimilivu wetu na kutotetereka katika kuifanya Serikali iwajibike kwa ahadi zake! Hatuwezi kuvumilia kuachwa nyuma tena.”

 

Maelezo kwa Wahariri:

Mapema mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitoa msaada wa nakala 1,000 za majarida yenye dondoo muhimu kuhusu Malengo ya Dunia yaliyochapishwa kwa nukta-nundu (braille)—yaani, ule mwandiko maalumu wa nukta ambao wenye uoni hafifu au kukosa uoni kabisa hutumia kusoma—kwa Seed Trust Tanzania ikiwa ni sehemu ya jitihada ya kuwafikia watu wenye matatizo ya kuona. Utoaji mafunzo kwa Mabingwa wapya 25 wa Malengo ya Dunia ni mwendelezo wa ushirika wa UN na SEED Trust, shirika ambalo linalenga kuleta uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi katika maisha ya Watanzania wenye ulemavu.

Seed Trust Tanzania ni shirika linaloshughulikia watu wenye ulemavu nchini likilenga kulinda na kuhamasisha haki za watu wenye ulemavu (za Waume kwa Wake) na pia kuongeza upatikanaji wa fursa za kijamii. Hii inadhihirishwa na tamko lake la msingi kuhusu mkazo katika utetezi, afya, elimu jumuishi, maisha na huduma za kufanya marekebisho kwa watu wenye ulemavu hapa nchini Tanzania.

Takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kwamba ifikapo mwaka 2014, zaidi ya asilimia 9 ya Watanzania watakuwa ni wenye ulemavu. Serikali inatenga asilimia 2 ya bajeti za manispaa katika kuelekea kwenye kuwaunga mkono watu wenye ulemavu.

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhari walisiana na:

Hoyce Temu                                                                           

Mtaalamu wa Mawasiliano                                                                

Ofisi ya Mratibu Mkazi wa UN

UN Tanzania

Simu ya mkononi: +255 682262627

Wavuti:    http://tz.one.org

Facebook: http://www.facebook.com/UNTanzania

Twitter:   @UnitedNationsTZ , @Alvaro_UNTZ

 

Peter Charles

Mratibu wa Miradi wa Nchi

Seed Trust Tanzania

S.L.P 2146

Mkononi: +255 716064759

Simu: +255 23 2613944

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Skype:PCharls