Press Releases

Maadhimisho ya Siku Ya Wakunga Duniani

5 May, 2018

 

 

 

Ndugu wanahabari

Tarehe 5 ya mwezi Mei kila mwaka dunia huadhimisha siku ya wakunga duniani. Maadhimisho ya Siku hii yana ongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA) na wadau wengine wa afya ya mama na mtoto.

Madhumuni ya maadhamisho haya ni kutoa hamasa kwa watunga sera na watoa maamuzi ili kuhakikisha kwamba rasilimali muhimu zinakuwepo kwa ajili ya wakunga lakini pia kutambua nafasi ya pekee waliyo nayo wakunga wenye taaluma katika jamii.

Ndugu Wanahabari

Vifo vya kina mama vimeripotiwa kupungua kwa asilimia 44 ulimwenguni, tangu mikakati ya kupunguza vifo ilipoanza miaka 25 iliyopita (1990-2015). Kumekua na mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano, hata hivyo bado tuna changamoto nyingi zinazohitaji kupewa kipaumbele ili tufikie malengo endelevu.

Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wanawake 303,000 wameendelea kupoteza maisha wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua (2015) na pia takribani watoto million 2.6 walipoteza maisha wiki chache baada ya kujifungua kwa mwaka 2016, Hii inamaanisha watoto wachanga 7,000 walipoteza maisha kila siku.  Asilimia 99% ya vifo hivi vinatokea katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania (WHO Maternal Mortality Fact Sheet 2016).

Ndugu wanahabari,

Ripoti ya hali ya wakunga duniani ya waka 2014 inasisitiza umuhimu wa uwepo wa wakunga wataalamu na upatikanaji wa huduma za wakunga wenye taaluma ili kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga. Kuna upungufu wa wakunga takribani millioni 9 duniani, hasa katika nchi za Kusini mwa bara la Asia na Afrika. Inakadiriwa kuwa utakuwepo uhitaji mkubwa wa wakunga wataalamu takribani millioni 14 ifikapo 2030 katika nchi za Kusini mwa bara la Asia na Afrika (WHO Global Strategy, 2016

Wakunga wataalamu wanao uwezo wa kutoa huduma bora ya afya ya uzazi inayojumuisha utunzaji wa mama na mtoto katika kipindi chote cha ujauzito hadi kujifungua. Hivyo basi,ni muhimu kuwa na mfumo na sera ya uuguzi unaoweka mazingira ya kazi yenye kuridhisha ili kuhakikisha wakunga waliopata mafunzo wanapangiwa na kubakia sehemu ya kazi iliyo sahihi.

Ndugu Wanahabari

UNFPA Tanzania imeendelea kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Afya Kitengo cha Uuguzi na Ukunga (DNMS) na chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kufanikisha yafuatayo:

  • Ukarabati wa vituo (8) vya afya zikiwemo wodi za kuzalishia na vyumba vya upasuaji kwa mikoa ya kanda ya ziwa ili viweze kutoa huduma za haraka za upasuaji (EmONC).
  • Ununuzi wa vifaa na mashine mbalimbali za kumwezesha mkunga kutoa huduma bora ya mama na mtoto.
  • Kuwajenga uwezo wa wakunga ili waweze kutoa huduma za dharura kwa mama na mtoto (EmONC) -  Jumla ya wakunga 76 wamepata mafunzo ya BEmONC (huduma za dharura kwa mama na mtoto ngazi ya dispensary) na 40 wamepata mafunzo ya CEmONC (huduma za dharura za upasuaji) kutoka Zanzibar, Newala na Nachingwea; na
  • Kuwezesha mapitio ya sera 3 za uuguzi na ukunga (nursing and midwifery national policies), kuboresha elimu ya uuguzi na ukunga kupitia ukarabati na ununuzi wa vifaa (skill lab) vya mafunzo ya kinadhari kwenye chuo cha uuguzi na ukunga Newala.

Ndugu Wanahabari

Kukua kwa uchumi kunategemea sana afya za wananchi wake; hivyo basi jamii inahitaji kutambua mchango wa wakunga na kuthamini kazi zinazofanywa na wakunga. Wakunga hutoa elimu ya afya inayohusu madhara ya ndoa za utotoni, tohara kwa watoto wa kike, kutoa huduma za uzazi wa mpango,kutibu magonjwa ambukizi yatokanayo na kujamiiana bila kinga (VVU na mengineyo) na huduma nyingine zinazohusu afya ya uzazi katika ngazi ya jamii kwa wakishirikiana na wanawake na familia zao.

Ili tuweze kufanikiwa, Serikali kupitia wizara ya afya kitengo cha uuguzi na ukunga, taasisi na wadau mbalimbali wa mashirika yasiyo ya kiserikali wa maswala ya mama na watoto hatuna budi kushirikiana kwa karibu na chama cha wakunga Tanzania, ili kuhakikisha kwamba tunaijenga kada ya wakunga wenye taaluma inayokubalika  kitaifa na kimataifa kwa faida ya  Taifa letu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mkunga ni kiongozi katika utoaji wa huduma bora kwa mama na mtoto” (“Midwives leading the way with quality care”)

Ahsanteni.