Press Releases

Ubalozi wa Norway waongeza msaada wake kwa Mpango wa UN Tanzania Moja kwa Dola za Marekani milioni 5.1

Ubalozi wa Norway waongeza msaada wake kwa Mpango wa UN Tanzania Moja kwa Dola za Marekani milioni 5.1

Eneo la Mkazo: Lengo la 2 – Kuondoa Njaa Kabisa & Lengo la 5 – Usawa wa Jinsia

 

06 Desemba 2017, Dar es Salaam – Ubalozi wa Norway leo umewekeana saini makubaliano na Mpango wa Umoja wa Mtaifa Tanzania ambapo umeongeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 5.1 katika makubaliano ya Mpango wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP II). Mchango jumla kutoka Norway kupitia UNDAP II ni kiasi cha Dola za Marekani milioni 10.5.

Makubaliano hayo yalitiwa saini rasmi wakati wa tukio lililofanyika katika Ubalozi wa Norway jijini Dar es Salaam kati ya Balozi wa Norway, Mh. Hanne-Marie Kaarstad na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Alvaro Rodriguez.

Msaada wa nyongeza utatolewa kwa madhumuni ya kuendeleza kilimo chini ya Mpango Kabambe wa Pamoja wa Kigoma, na vilevile ili kupanua msaada kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa ili kumaliza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mh. Hanne-Marie Kaarstad, alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania za kutoa hifadhi kwa takribani wakimbizi 340,000 katika Mkoa wa Kigoma. “Serikali ya Tanzania imeomba msaada kutoka kwa washirika wa maendeleo kuwaletea mabadiliko yenye tija jamii za wenyeji na kuleta matokeo yanayokwenda zaidi ya kukidhi mahitaji ya haraka ya kiutu.  Msaada wa fedha kutoka Norway kupitia Mpango Kabambe wa Pamoja wa Kigoma ndiyo mwitikio wetu kwa ombi lile.”

Vilevile, Balozi Kaarstad alifafanua kwamba nchi ya Norway ni mwungaji mkono wa muda mrefu katika masuala ya haki za wanawake. Msaada wa Norway kupitia UNDAP II umewawezesha wanawake kupata mafunzo ya ujasiriamali, na pia kuchangia katika juhudi za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Balozi Kaarstad aliwekea msisitizo msaada kwa Umoja wa Mataifa: “Tunaamini Umoja wa Mataifa unapotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja unaleta matokeo bora mahali unapofanya kazi kwa manufaa ya Watanzania wote.”

Kwa upande wake, Bw. Rodriguez aliishukuru Serikali na watu wa Ufalme wa Norway kwa misaada yake akieleza kwamba Norway imekuwa mshirika imara wa maendeleo kwa shughuli za Umoja a Mataifa kwa Tanzania. “Kwa miongo mingi, Norway imeendelea kuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Umoja wa Mataifa. Kwa kuweka mkazo katika mahitaji ya wanawake na watoto walio hatarini, rasilimali hizi zitatoa mchango muhimu katika kukidhi mahitaji ya wale ‘walio nyuma sana’ kama inavyoelezwa katika Malengo ya Dunia. Kwa kuongezea, Bw. Rodriguez alieleza kwamba Umoja wa Mataifa Tanzania unashauku ya kuimarisha ushirika na Norway katika miaka ijayo ili kuwasaidia watu wa Tanzania, waume, wake na watoto kuendeleza vipawa vyao vya kujitegemea kikamilifu.

Mchango wa Norway utatolewa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa, ambao ulianzishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini ili kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa wa 2016-2021 (UNDAP II).

 

Matini/Maelezo kwa Wahariri:

Mwaka jana Norway ilitoa mchango wa takribani Dola za Marekani milioni 4.8 (sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 10.6).  Mchango wa nyongeza unajazia takribani Dola za Marekani milioni 5.1 (sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 11.4).

 

Norway na Umoja wa Mataifa Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri wa kiushirika wa muda mrefu ambapo nchi hiyo imetoa hapo kabla mchango wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 16 kupitia Mfuko wa Pamoja katika mzunguko wa kwanza wa programu – UNDAP I (2011-2016). Mchango huu wa sasa wa Norway utasaidia Umoja wa Mataifa Tanzania katika programu yake mpya iliyozinduliwa hivi karibuni, UNDAP II (2016-2021).

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Victor Mlunde

Ofisa Programu

Masuala ya Utawala na Siasa

Ubalozi wa Norway, Dar Es Salaam

Simu ya mkononi: +255 782 777013/ +255 714 289428

Ofisi: +255 222 163 100

www.norway.go.tz– Facebook

 

Hoyce Temu                                                                                       

Mtaalamu wa Mawasiliano                                                                   

Ofisi ya Mratibu Mkazi, Umoja wa Mataifa Tanzania

Simu ya Mkononi: +255 682262627

Wavuti:    http://tz.one.org

Facebook: http://www.facebook.com/UNTanzania

Twitter:    @United NationsTZ, @Alvaro_UNTZ

-30-