Press Releases

Ubalozi wa Uswidi (Sweden) watoa Dola za Marekani milioni 36 kwa Umoja wa Mataifa

TAARIFA YA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI  

Ubalozi wa Uswidi (Sweden) watoa Dola za Marekani milioni 36 kwa Umoja wa Mataifa

Maeneo yanayolengwa: Wanawake, watoto, vijana kuwa miongoni mwa wanufaika

 

Imezuiwa hadi adhuhuri ya tarehe 30 Oktoba

 

30 Oktoba, Dar es Salaam – Ubalozi wa Uswidi nchini Tanzania umewekeana saini makubaliano na Umoja wa Mataifa Tanzania ambapo Uswidi itatoa jumla ya Dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo. Makubaliano hayo yametiwa saini rasmi leo na Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez, katika ofisi za Ubalozi wa Uswidi jijini Dar es Salaam. Mchango wa Uswidi utasaidia jitihada za Umoja wa Mataifa za kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi ulio jumuishi na ajira na kuimarisha utawala wa kidemokrasi, haki za binadamu na usawa wa jinsia. Mchango huo pia utasaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akifafanua utayari wa dhati wa Uswidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, Balozi Rangnitt alieleza kwamba Uswidi imechagua kusaidia shughuli za Umoja wa Mataifa zinazoakisi malengo ya maendeleo ya nchi katika nyanja za haki za wanawake, utawala wa demokrasia na ukuaji wa uchumi. Shughuli hizo ni zile zinazomnufaisha kila mmoja katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa kipato cha kati. “Kwa kupitisha sehemu ya msaada wetu kupitia Mfuko wa Umoja wa Mataifa chini ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja, tunashiriki kikamilifu katika kusaidia ufikiwaji wa malengo ya maendeleo ya Tanzania. Vilevile, tunatambua bayana kabisa na kuthamini wajibu uliokubaliwa kuwa ndio wa Umoja wa Mataifa katika kuleta maendeleo endelevu. Kwa msaada huu, tunawezesha uchukuaji hatua unaoendana na sera ya nje inayozingatia haki za wanawake ya Uswidi na pia jitihada zinazolenga, miongoni mwa mambo mengine, ajira yenye hadhi na haki za watoto. Hii inadhihirisha mwendelezo wa uhusiano wa karibu na Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania wenye lengo la kuleta maendeleo yenye usawa na jumuishi zaidi,” alisema Balozi.

Akisisitiza utayari wa kuendelea kuisaidia Tanzania na Umoja wa Mataifa, Balozi alitumia fursa hiyo kuthibitisha kuyapokea kwa moyo mmoja mageuzi ya Mfumo wa UN chini ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja na kutambua njia fungamanifu zinazotumika na thamani inayopatikana kutokana na mchango wa mashirika ya UN katika lengo moja kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, washirika wa kijamii na vyama vya kiraia.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Rodriguez alitoa shukrani kwa serikali na watu wa Uswidi kwa msaada wao endelevu akiipongeza Uswidi kwa kuwa mshirika wa maendeleo asiyeyumba katika shughuli za Umoja wa Mataifa Moja na pia kwa Tanzania. “Uswidi imekuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Umoja wa Mataifa kwa miongo mingi. Kwa kulenga wale walio wanyonge kabisa katika jamii hii, rasilimali hii itatoa mchango muhimu sana katika kushughulikia mahitaji ya wale ‘walio chini sana’ kama inavyoelekezwa katika Malengo ya Ulimwengu,” alisema.“Mchango huu utauwezesha Umoja wa Mataifa kuweza kufanya kazi katika masuala mapana mengi kama vile kuhamasisha fursa za ajira zenye hadhi kwa Watanzania maskini, kuendeleza kanuni za utawala bora, na nafasi ya uongozi wa wanawake katika masuala ya siasa na vilevile kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” aliongeza.

Matini (maelezo) kwa Wahariri:

Mchango wa Uswidi utapokelewa kupitia Mfuko Mmoja wa Tanzania, ambao ni mfuko ulioandaliwa rasmi kwa ajili ya mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini ili kutekeleza Mpango wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa wa 2016-21 (UNDAP II). Tangu Mfuko Mmoja (chini ya Mpango wa Kufanya Kazi pamoja) ulipoanza kufanya kazi mwaka 2007, Uswidi imechangia Dola za Marekani milioni 29.2.

Katika eneo la ukuaji wa kiuchumi ulio jumuishi, ambao utatengewa Dola za Marekani milioni 15, mchango wa Uswidi utayawezesha mashirika ya Umoja wa Mataifa kusaidia biashara za ndani zilizo kwenye uzalishaji na zenye mnyororo wa thamani unaotekelezeka na ulio jumuishi na wenye uwezekano wa kutengeneza ajira, hasa kwa wanawake na vijana, na kuhakikisha ushiriki wa uhakika na wenye kuleta tija kwenye uchumi.

Eneo la Utawala wa Kidemokrasi na Haki za Binadamu litatengewa Dola za Marekani milioni 10. Fedha hizi zitasaidia jitihada za Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kuimarishwa kwa utawala wenye ufanisi, ulio wa wazi, wenye uwajibikaji na ulio jumuishi. Kwa kuongezea, fedha hizo zitasaidia kuongeza ubora wa kazi za Kibunge, kupatikana kwa huduma bora katika mfumo wa utoaji haki kwa raia na kusaidia vyombo vya haki za binadamu vya serikali kutimiza wajibu wao kikamilifu. Fedha hizi pia zitashughulikia kazi zinazokazia usalama na kinga kwa waandishi wa habari na kuimarisha utendaji kazi wa redio za ndani ili kuongeza upatikanaji wa habari bora kwa wanajamii.

Jumla ya Dola za Marekani milioni 12 zitatumika katika programu zinazowalenga wanawake na watoto kupitia shughuli zinazohamasisha ushiriki wa wanawake katika siada na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto (VAWC). Miongoni mwa shughuli nyinginezo, juhudi katika eneo hili zinalenga kuongeza idadi wa wanawake wanaoingia katika kuwania nafasi za uongozi wa kuchaguliwa. Kazi ya kuzuia VAWC itaimarishwa kupitia uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa Taifa wa miaka mitano wa Kukomesha Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA).

-30-

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

 

 

Bi. Charlotte Compton

Ofisa mawasiliano na utawala

Ubalozi wa Uswidi jijini Dar es Salaam

Simu: +255 684 503 922

Ofisi: +255 22 219 6533

Wavuti: swedenabroad.com/en-GB/Embassies/Dar-es-Salaam/

Facebook:Embassy Of Sweden In Dar Es Salaam

Twita: @SwedeninTZ

 

 

Bi. Hoyce Temu                                                                                            

Mtaalamu wa Mawasiliano                                                                

Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania

Simu: +255 682 262 627

Wavuti:    http://tz.one.org

Facebook: United Nations Tanzania

Twita:    @UnitedNationsTZ, @Alvaro_UNTZ

Instagram: @unitednations_tz