HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. KASSIM M. MAJALIWA, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA NNE WA MWAKA WA KUTATHMINI AFUA ZA LISHE NCHINI

HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. KASSIM M.  MAJALIWA, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA NNE WA MWAKA WA KUTATHMINI AFUA ZA LISHE NCHINI TAREHE 6 SEPTEMBA, 2017

 

 

 • Mheshimiwa Ummy Mwalimu(Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;

 

 • Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango;

 

 • Mheshimiwa Selemani Jaffo (Mb.), Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI;

 

 • Mheshimiwa Peter Mavunde, (Mb.) Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana;

 

 • Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ndugu Jordan Rugimbana; pamoja na viongozi wengine wa ngazi za Mkoa na Halmashauri mliopo;

 

 • Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Vyama vya Siasa mliopo mahali hapa;

 

 • Waheshimiwa Mabalozi Mnaoziwakilisha nchi mbalimbali;

 

 • Viongozi waandamizi wa Idara, Taasisi, Wakala za Serikali, na Wakuu wa Vyuo vya Elimu ya Juu;

 

 • Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia;

 

 • Dkt. Joyceline Kaganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania;

 

 • Ndugu Wageni Waalikwa, Waandishi wa habari na wadau wote wa Lishe; Mabibi na Mabwana;

 

Habari za jioni.

 

1.0        UTANGULIZI – SHUKRANI:

 

·         Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukusanyika mahali hapa siku ya leo kwa ajili ya shughuli hii muhimu. Nitumie fursa hii pia kukushukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu(Mb.) na uongozi mzima wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushiriki kwenye tukio hili muhimu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Nawashukuru pia wadau wote wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi, viongozi wa Serikali kutoka katika ngazi mbalimbali waliokuja kushiriki pamoja nasi.

 

·         Kwa namna ya kipekee napenda pia kutumia fursa hii kuwatambua na kuwashukuru wadau ambao walijitolea kwa hali na mali hadi kuwezesha kufanyika kwa mkutano huu. Wadau hao ni Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO, WFP, FAO, UN-REACH na UNICEF; Mashirika hisani ya USAID na Irish Aid; na Mashirika yasiyo ya kiserikali ya Mwanzo Bora, Nutrition International na Hellen Keller International.

 

·         Aidha, napenda pia kutumia fursa hii kuungana na waliotangulia kuwakaribisha Dodoma, Makao Makuu ya Tanzania; wageni wetu wote hasa wale waliotoka nje ya Mkoa wa Dodoma na nje ya nchi kuja kushirikiana nasi katika mkutano huu muhimu. Karibuni sana Dodoma na karibuni sana Tanzania.

 

2.0        UMUHIMU WA MKUTANO HUU:

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni waalikwa Mabibi na Mabwana;

·         Siku ya leo ni siku muhimu sana, kwani tumekusanyika hapa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini; utekelezaji unaojumuisha wadau mbalimbali wa kisekta kwa kuwa sote tunafahamu na kujiridhisha kuwa lishe ni suala mtambuka na wote tunatakiwa kuwekeza kwenye lishe. Hivyo, mafanikio katika harakati za kudhibiti utapiamlo nchini yanategemea kuunganisha nguvu zetu.

 

·         Nimearifiwa kwamba mkutano huu hufanyika kila mwaka na hii ni mara ya nne kufanyika tangu utaratibu huu uanze ambapo wadau wote wa chakula na lishe nchini kujumuika na kutathmini utekelezaji wa masuala ya lishe.  Wadau hao ni pamoja na Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia, Sekta binafsi, Wataalamu wa Chakula na Lishe kutoka ngazi za Mikoa Halmashauri na Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti. Kusanyiko hili linaonesha jinsi suala la chakula na lishe linavyomgusa kila mmoja wetu katika nafasi yake japo kwa njia tofauti. Ninawapongeza sana waandaaji wa mkutano huu kwa kutuleta pamoja bila kujali tofauti zetu za kimajukumu au kitaaluma; tukiwa na lengo moja tu la kuondokana na utapiamlo nchini.

 

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni waalikwa Mabibi na Mabwana;

·         Sote tutambue kwamba maendeleo ya Taifa letu, pamoja na mambo mengine, yanahitaji watu wenye afya njema na hali bora ya lishe. Ili tuwe na watu walio na hali bora ya lishe, tunapaswa kuwa na uelewa wa kina wa kitu gani kinasababisha lishe duni katika kila eneo la nchi yetu na kubuni mikakati ya kukabiliana na aina zote za utapiamlo katika jamii zetu. Jambo hili litafanikiwa endapo elimu sahihi ya lishe itatolewa na kuimarisha ushiriki wa kila sekta, kila mdau na kila mtu katika nafasi yake.

·         Jambo hili la ushiriki wa kila sekta nimekuwa nikilisisitiza mara kwa mara na kwa uzito mkubwa zaidi ndiyo sababu Serikali inatoa kipaumbele cha kutosha katika masuala ya lishe kwa Jamii.

 

·         Nakubaliana na Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa lishe duni inachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri afya ya jamii yetu hususan ya watoto na akinamama. Lishe duni siyo tu inaathiri maendeleo ya ukuaji wa watoto wetu kimwili na kiakili, bali pia ni chanzo cha kupungua kwa tija katika nguvu kazi ya Taifa.  Lishe duni huongeza gharama za matibabu kutokana na kuongezeka kwa magojwa ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza kama vile kisukari na magonjwa ya moyo, ambayo husababishwa na ulaji duni na mtindo wa maisha usiofaa.

 

·         Wataalam wanatueleza kwamba athari azipatazo mtoto aliyedumaa katika kipindi cha siku 1,000 za kwanza za uhai wake, hazirekebishiki. Hivyo, ni jambo lisilopingika kuwa utapiamlo ni kiashiria kimojawapo cha umasikini katika kaya na kwa kiasi kikubwa unachangia katika kupunguza kasi ya maendeleo ili kufikia malengo endelevu ya maendeleo hapa nchini.

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni waalikwa Mabibi na Mabwana;

·         Uboreshaji wa lishe ni mojawapo ya vipaumbele katika kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo, kupunguza vifo vya watoto wachanga na wadogo, kuboresha afya ya mama mzazi pamoja na kutokomeza umaskini na njaa. Wataalam wanatuambia kuwa watoto waliopata huduma bora za lishe hasa katika kipindi cha siku 1,000 za kwanza za uhai wao, yaani tangu mama anapopata ujauzito hadi mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili wanapata faida zitakazodumu katika maisha yao yote.

 

·         Baadhi ya faida za makuzi mazuri kwa mtoto ni pamoja na;  maendeleo mazuri ya ukuaji wa ubongo,  uwezo mzuri wa kukabiliana na maradhi, uwezo mzuri kiakili (higher IQ), uwezo na ufanisi wa kujifunza na uwezo mkubwa wa kujiingizia kipato wakiwa watu wazima. Matokeo ya hali hizi ni kuwasaidia katika kukwamua nchi zao kutoka kwenye umaskini na kuleta maendeleo. Uwekezaji katika lishe pia unasaidia kuinua Pato la Taifa kwa asilimia 2 hadi 3 kila mwaka.

 

·         Aidha, wataalam wa uchumi wanatuambia kuwa utoaji wa vitamini na madini kwa watoto chini ya miaka mitano ni mkakati mzuri zaidi wa uwekezaji katika lishe. Kila dola moja ya Marekani ($1 sawa na sh. 2,220) inayowekezwa kwenye watoto kupitia mkakati huu utakuja kupata faida ya dola za Marekani thelathini ($30) hapo baadaye, hiki ni kiwango kikubwa kabisa cha faida katika uwezekaji wa aina yoyote.

 

·         Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwa na lishe bora na katika moja ya hotuba zake zaidi ya miaka kama 30 iliyopita.  Aliwahi kusema hivi:

“....nimeongelea kwa kirefu kuhusu suala la chakula kwani ndiyo msingi wa maendeleo ya watu. Mtu anayeumwa na njaa hawezi kufanya kazi na kuleta maendeleo, kwani ni mdhaifu wa mwili na pia ni mdhaifu kiakili”.  (Mwisho wa kunukuu).

 

Mwalimu Nyerere alisisitiza kukumbuka jambo hili kama la lazima    hususan pale lishe ya watoto inapohusika. Alisema hivi:

 

“Mtoto anapokuwa hajalishwa vizuri hawezi kukua vizuri kwani ataathirika kiafya na pia akili yake, na hataweza kufikia uwezo wake kamili wa kufanya vizuri shuleni na baadaye kushiriki kikamilifu katika kuzalisha mali na kujenga uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo suala la chakula cha kutosha, na kilicho na lishe-bora ni suala la msingi kabisa kwa maendeleo ya watu mijini na vijijini”. (Mwisho wa kunukuu).

 

3.0 DHAMIRA YA SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HALI YA CHAKULA NA LISHE KAMA MSINGI WA MAENDELEO

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni waalikwa Mabibi na Mabwana:

·            Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwekeza katika lishe kama mkakati mmojawapo wa kufanikisha azma ya Serikali kufikia uchumi wa kipato cha kati na viwanda ifikapo 2025. Baraza la Umoja wa Mataifa limetoa azimio la kuwa kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2025 ni miaka ya “Kuchukua Hatua katika Kutekeleza Masuala ya Lishe - Decade of Action on Nutrition”.

 

·            Msisitizo katika kipindi hiki ni kuongeza fursa ya kuunganisha juhudi za wadau kuboresha hali ya chakula na lishe kupitia sekta mbalimbali. Vilevile, Serikali kwa upande wetu, tunatambua kuwa hata katika kuyafikia Malengo Endelevu ya Maendeleo (Sustainable Development Goals), lishe ni moja ya mhimili muhimu wa kuwezesha kufikiwa kwa malengo yote 17.

 

·            Hivyo basi, niendelee kuwahakikishia kwamba uwepo wangu kwenye mkutano huu, unadhihirisha utayari wa Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote kushiriki katika kuchangia jitihada za kupambana na utapiamlo. Kwa kufanya hivi, tutaweza kuimarisha mikakati yetu ya kuivusha nchi yetu na watu wake kutoka katika lindi la umaskini na kujenga nguvu kazi imara itakayoweza kuhimili changamoto za maendeleo ya viwanda.

 

·            Nitumie fursa hii kuwasihi wadau wengine kote nchini, waendelee kutuunga mkono kwa kuwekeza kwenye utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ambayo inalenga kuboresha hali ya chakula na lishe miongoni mwa jamii; hasa watoto, wanawake walio katika umri wa kuzaa, vijana na watu wenye mahitaji maalum kilishe.

 

3.0        HITIMISHO

 

Wadau mliopo, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;

·                Nimefurahishwa sana na kaulimbiu ya mkutano huu isemayo “Lishe Bora: Msingi wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania” ambayo kimsingi inaendana na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Napenda kuwahamasisha wadau wawekeze kwenye viwanda vya usindikaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kuongeza wingi wa vitamini na madini katika vyakula na hatimaye kuboresha lishe na afya ya jamii. Napenda kusisitiza kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo tutumie fursa hii kikamilifu.

 

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

 

·            Pamoja na heshima mliyonipa ya kufungua mkutano huu mmeniomba nizindue rasmi Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe. Nimefahamishwa kuwa maandalizi ya mpango huu yameshirikisha wadau wote wa lishe na yalizingatia pia maeneo ya kimkakati katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2016/17 - 2020/21 na utekelezaji wake utahusisha wadau wote wa kisekta; ndani na nje ya Serikali.

 

·            Aidha, mpango huu umeonesha majukumu ya kila mmoja na gharama zinazohitajika kutekeleza mikakati hiyo ya lishe. Ninawaagiza watendaji wakuu wote katika Wizara husika, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, wahakikishe mpango huo unatekelezwa ipasavyo na kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.  Vivyo hivyo, Wakuu wa Mikoa na Wilaya mhakikishe mnaisimamia Mikoa na Halmashauri zenu kutekeleza afua zilizoainishwa katika mpango huu kwa kuzijumuisha katika Mipango yenu na kuzitengea fedha kwenye bajeti zenu kila mwaka.

 

·            Vilevile, nasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote, wahakikishe Shilingi 1,000 ambazo Halmashauri zilielekezwa kutenga kwenye bajeti kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya kuboresha lishe kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, zinatolewa na kutumika kama ilivyopangwa. Aidha, kila mdau wa lishe nchini aonyeshe bayana mchango wake katika kukabiliana na utapiamlo nchini. Viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali wabaini kiwango cha utapiamlo katika maeneo yao, waonyeshe mbinu za kukabiliana na hali hiyo, wafanye tathmini ya ufanisi na watoe taarifa za ufanisi.

 

·            Mwisho, Wizara ya Afya, ihakikishe inaharakisha mchakato wa kuweka virutubishi muhimu vyote (Essential nutrients) na chakula dawa (F75, Resomal, F100 na Plumpy nuts) katika Mpango wa Taifa wa Dawa Muhimu (Essential Drugs List) pamoja na vifaa tiba vya lishe. Kukamilika kwa mchakato huu, kutawezesha hospitali zote kuagiza virutubishi na dawa hizi muhimu kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Serikali imeshaweka mazingira mazuri ya kuwezesha utekelezaji wa afua za lishe, ikiwa ni pamoja na sheria, kusamehe kodi ya bidhaa na mashine zilizoainishwa kusaidia uwekezaji kwenye lishe hasa kwa Afya ya Mama na Mtoto.

 

Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

·            Naomba kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena waandaaji wa mkutano kwa kunialika kwenye ufunguzi wa mkutano huu muhimu. Shukrani zangu pia ziwafikie wadau wote waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huu hapa Dodoma kwa kutoa mchango wao wa fedha, vifaa au hata kwa mawazo. Nipende kuwathibitishia kuwa Serikali inatambua mchango wenu na itaendelea kudumisha ushirikiano uliopo kwa manufaa ya Watanzania wote.

 

Mabibi na Mabwana;

·            Baada ya kusema hayo sasa napenda kutamka kuwa Mkutano wa Nne wa Wadau wa Masuala ya Lishe nchini umefunguliwa rasmi na sasa nipo tayari kufanya uzinduzi wa mpango wa Taifa wa utekelezaji wa masuala ya lishe kwa utaratibu ulioandaliwa.

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MUNGU WABARIKI WATOTO WA TANZANIA

 

Asanteni kwa kunisikiliza.