Press Releases

MAADHIMISHO YA 72 YA UMOJA WA MATAIFA

TAARIFA YA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Imezuiwa hadi Oktoba 24 saa sita mchana kwa saa za Afrika Mashariki

 

MAADHIMISHO YA 72 YA UMOJA WA MATAIFA

 

“Maendeleo ya Viwanda, Utunzaji Mazingira kwa Maendeleo Endelevu”

 

Oktoba 24, 2017 Dar es Salaam – Umoja wa Mataifa husherekea kuanzishwa kwake kila ifikapo Oktoba 24. Mfumo wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Serikali, washirika wa maendeleo na vijana umeadhimisha miaka 72 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika viwanja vya Karimjee na na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Siku ya Umoja wa Mataifa mwaka huu imebeba Ujumbe unaohusiana na utunzaji wa mazingira “Maendeleo ya Viwanda na Utunzaji wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu”. Maadhimisho hayo kwa upande wa Zanzibar yatafanyika tarehe 26 Oktoba.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu Mkazi wa UN na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Alvaro Rodriguez, alikazia mafanikio yaliyopatikana chini ya Mpango wa Kwanza wa Umoja wa Mataifa wa Msaada wa Maendeleo (UNDAP I - 2011 hadi 2016) na vile vile utekelezaji wa mapema wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Msaada wa Maendeleo (UNDAP II - 2016 hadi 2021) unaoweka mkazo katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na mipango ya maendeleo ya taifa kwa upande wa Bara na Zanzibar.

 

Vile vile, Bw. Rodriguez aliangazia Programu Kamambe ya Pamoja ya Kigoma, ambayo hivi sasa inafadhiliwa na Norway na KOICA, ambayo imebuniwa maalumu ili kukidhi vipaumbele vya maendeleo vya Mkoa wa Kigoma na hasa kwa kuzilenga jamii za wenyeji Watanzania katika wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na Kakonko, ambazo kwa pamoja zinawahifadhi zaidi ya wakimbizi 300,000.

 

Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu, Mh. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ya Tanzania kwa kipindi kirefu. Mh. Makamu wa Rais alisisitiza,  “Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu, Maendeleo ya Viwanda na Utunzaji Mazingira kwa Maendeleo Endelevu, unaendana vema kabisa na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 na Awamu ya Pili ya Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano unaoanzia2016/2017 hadi 2020/2021, unaokusudiwa kuishajiisha Tanzania kuingia katika uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.”.

 

Makamu wa Rais pia alitoa wito kwa Timu ya Uongozi ya Umoja wa Mataifa Nchini (UNCT) kuunganisha mafanikio yaliyokwishapatikana kupitia utekelezaji wa UNDAP I na UNDAP II unaoendelea kutekelezwa.

 

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 72 ya Umoja wa Mataifa, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Alvaro Rodriguez, aliongeza: “Tanzania na Umoja wa Mataifa zimekuwa na uhusiano mzuri wa ushirikiano kwa miongo mingi. Wakati Tanzania inapitia mabadiliko makubwa hasa kuelekea katika hadhi ya kipato cha kati, msaada wa Umoja wa Mataifa hauna budi kukidhi mahitaji na changamoto mpya ambapo ni lazima itoe maana mpya kwa dhima yake katika Tanzania ambayo ni changamani, ya vijana na iliyo motomoto”.

 

Matini/Maelezo kwa Wahariri:

Umoja wa Mataifa ulianza kazi zake mnamo Oktoba 24, 1945. Kwa hiyo, unatimiza miaka 72 tangu kuanzishwa kwake.

Mwaka huu ni wa pili katika utekelezaji wa UNDAP II huku mkazo ukiwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, uhifadhi wa mazingira na viwanda, na programu mahalia iliyozinduliwa hivi karibuni kwa ajili ya mkoa wa Kigoma, ‘Programu Kamambe ya Pamoja ya Kigoma’, ambayo itatekelezwa kati ya 2016-2021 katika wilaya tatu (Kasulu, Kibondo na Kakonko) kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya jamii za wenyeji za Watanzania.

Katika mwaka huu pia Umoja wa Mataifa ulishuhudiwa ukianzisha ushirikiano na sekta binafsi kupitia Fursa ili kuwafikia vijana kote nchini kwa ujumbe tofauti wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu utoaji kipaumbele kwa SDGs nchini Tanzania.

 

Kwa taarifa zaidi kuhusu Wiki ya Umoja wa Mataifa, tafadhali wasiliana na:

Bi. Mindi Kasiga – Mkuu wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje (This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.)

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (MOFAEAC) 0784 777606

Bi. Hoyce Temu, Mtaalamu wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa Tanzania (This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.) - 0682262627