Press Releases

WFP Yaanza Utekelezaji Wa Mpango Mkakati Mpya Nchini Tanzania

 

 

 

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

 

25 Julai 2017

 

WFP YAANZA UTEKELEZAJI WA MPANGO MKAKATI MPYA NCHINI TANZANIA

 

DAR ES SALAAM –Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limezindua Mpango Mkakati wa Nchi (CSP) wa Tanzania utakaodumu kwa miaka minne. Mpango huu unaendana kikamilifu na Ajenda ya UN ya 2030 ya Maendeleo Endelevu inayolenga kuondoa umaskini, kupunguza tofauti ya usawa, kukabili mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhakikisha kunakuwa na kilimo endelevu na usalama wa chakula.

 

Kupitia CSP, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linakusudia kuimarisha uwezo wa kupata soko kwa wakulima wadogowadogo 250,000 wakati likisimamia programu ya lishe inayohusisha sekta mbalimbali kwa akina mama 185,000 na akina mama wanaonyonyesha na watoto wa umri wa chini ya miaka miwili, na kutoa msaada wa chakula kwa zaidi ya wakimbizi 300,000.

 

“Utayarishaji wa Mpango Mkakati mpya wa Nchi wa WFP unaipa Serikali fursa ya kuchagua maeneo ya kipaumbele ambako, pamoja na washirika wetu, tunaweza kupunguza taathira ya majanga kwa watu walio hatarini ili waweze kujinusuru na kujiletea usalama zaidi wa chakula,” anasema Brigedia Jenerali Mbaazi Msuya, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

Kwa namna ya pekee, WFP inalenga malengo mawili katika 17 yaliyokubaliwa kote ulimwenguni ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs): SDG2 – Kuondoa Njaa Kabisa - na SDG17 – Kujenga Ushirika ili Kufikia Malengo. Lengo la 2 la SDG linakusudiwa kuondoa njaa hadi ifikapo mwaka 2030 wakati ambapo Lengo la 17 linahamasisha ushirika, kwa upande wa umma na ule wa binafsi.

 

“CSP inaweka msingi kwa ajili ya kazi za WFP nchini Tanzania wakati ikihakikisha kiwango cha juu cha thamani tunaposhirikiana na Serikali katika kufikia SDGs na hadhi ya kipato cha kati mwaka 2025,” anasema Michael Dunford, Mwakilishi wa Nchi wa WFP Tanzania. “Mpango huu mzima umebebwa kwenye miundodhana ya Serikali kuhusu maendeleo na dharura; inasaida kuimarishwa kwa mfumo kwa mtazamo wa kuelekea katika umiliki wa kitaifa.”

Mpango kazi huu wa Tanzania unaendeleza maeneo ambamo WFP ina weledi wa kutosha nchini. Shughuli kuu zinahusisha msaada kwa wakimbizi; programu teuzi za lishe; msaada kwa wakulima wadogowadogo; kujenga uwezo wa serikali na kutoa huduma za usambazaji wa vituo vingi; na kuanzisha kituo cha majaribio cha ugani, ili kuimarisha na kupanua ubunifu unaochangia kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

 

Mkazo mkubwa katika kazi za WFP unaendelea kuwa katika dharura na msaada wa chakula. Asilimia 85 ya bajeti ya Shirika ya miaka minne ya Dola za Marekani milioni 455.7 imetengwa kusaidia wakimbizi wapatao 310,000 pamoja na jamii za wenyeji kaskazini-magharibi mwa Tanzania.

 

Mpango Mkakati wa Nchi umesanifiwa ili kuwezesha uwekaji mipango wa muda mrefu ili kuunga mkono Mpango waPili wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP II) na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Serikali wa Miaka Mitano. Uliandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Tanzania, wahisani na washirika wengine wa maendeleo kufuatia uchambuzi wa kina, ikiwemo tathmini ya kimkakati inayojitegemea iliyofanywa na taasisi ya kitaifa ya utafiti katika masuala ya jamii na uchumi.

 

Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nchi kwa Tanzania ulianza tarehe 1 Julai, baada ya kupitishwa na Bodi Tendaji ya WFP mwezi Juni.

 

#                      #                      #

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ndilo shirika kubwa zaidi la misaada ya kiutu linalopambana na njaa kote ulimwenguni, likitoa msaada wa chakula kwenye maeneo yenye dharura na kushirikiana na jamii ili kuimarisha lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru. Kila mwaka, WFP inasaidia takribani watu milioni 80 katika nchi 80 ulimwenguni.

 

Kujua zaidi kuhusu WFP nchini Tanzania, soma: http://www1.wfp.org/countries/tanzania

 

Tufuatilie katika Twita: @wfp_tanzania and @wfp_media

 

Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Nchi wa WFP Tanzania umefanywa kwa ushirikiano na Clouds Media Group.

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

 

Fizza Moloo, WFP, This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it., simu. +255 (0) 759 686 543