Press Releases

Irish Aid & WFP Joint Press Release (Swahili)

Taarifa ya pamoja kwa Vyombo vya Habari 
 
1 Desemba 2016
 
IRELAND YASAIDIA KUENDELEZA MSAADA MUHIMU KWA WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA
 
DAR ES SALAAM – Leo, Serikali ya Ireland imelipa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mchango wa Euro 500,000 ili kusaidia wakimbizi wanaohifadhiwa nchini Tanzania. Kwa fedha hizi, Serikali ya Ireland inalisaidia Shirika la WFP kuendeleza operesheni za msaada kwa takribani wakimbizi robo milioni. Wakimbizi hawa, wengi wakitokea nchini Burundi, wanahifadhiwa na Serikali ya Tanzania katika kambi tatu mkoani Kigoma, magharibi mwa Tanzania.
 
Kutokana na kasi ya kuingia kwa wakimbizi—ambapo hivi sasa zaidi ya wakimbizi 10,000 wanavuka mpaka kuingia Tanzania kila mwezi—WFP imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa fedha kuendesha operesheni zake za kusaidia wakimbizi. Kwa sababu ya michango kutoka Serikali ya Ireland na wahisani wengine, hatari ya kupunguzwa kwa migao wanayopokea wakimbizi imeepushwa, walau hadi mwakani.
 
“Ireland imejitolea kwa dhati kabisa kupunguza njaa na utapiamlo kote duninani,” anasema Balozi wa Ireland Paul Sherlock. “Tanzania daima imeonyesha ukarimu mkubwa wa kuwapa hifadhi makundi makubwa ya wakimbizi. Ni matumaini yetu mchango wa leo utaisaidia serikali, WFP na washirika wake kuhakikisha kwamba mahitaji ya chakula kwa ajili ya wakimbizi walio hatarini zaidi wanaoishi nchini Tanzania yanakidhiwa.”  
 
Wakimbizi hupokea msaada muhimu wa chakula kilichopikwa katika vituo vya kuvukia na vya kupokelea, na mgao wa chakula cha mwezi katika kambi ambacho ni mahindi, kunde, chumvi, mafuta ya kupikia na uji uliowekewa virutubisho.
 
WFP vilevile inatoa chakula cha nyongeza kwa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha, watoto wa umri chini ya miaka mitano, wagonjwa waliolazwa hospitalini na watu wanaoishi na VVU/UKIMWI. Programu hizi za ulengaji maalumu huwapa wanufaikaji hawa lishe inayohitajika sana kupitia migao ya nyongeza ya chakula kilichoongezewa virutubisho. Virutubisho hivi vinaweza kuwa muhimu sana katika kupiga vita kudumaa na ukosefu wa lishe kwa watoto na wakati huohuo kimarisha mifumo ya kinga ya watu walio hatarini zaidi.
 
“Mchango huu unaoonyesha ukarimu mkubwa kutoka Serikali ya Ireland kwa kweli utaimarisha sana programu zetu za utoaji chakula na lishe kwa watu hawa waliokimbia makwao,” anasema Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania, Bwana Michael Dunford. “Hivi sasa tunaweza kuweka fikra zetu katika mahitaji ya chakula na lishe kwa kundi hili la wakimbizi linalozidi kukua kwa mwaka 2017.” 
 
Tanzania inaendelea kupokea mamia ya wakimbizi wapya kila siku. Hali ya ukosefu wa usalama nchini kwao inafanya kurejea kwao katika nchi hizo katika siku za usoni za karibuni kuwa jambo lisilo na uhakika. WFP inahitaji takribani dola za Marekani milioni 6 kila mwezi ili kuwasaidia wakimbizi. 
 
#                      #                      #
 
WFP ndilo shirika kubwa zaidi la misaada ya kiutu linalopiga vita njaa kote duniani, likitoa msaada wa chakula nyakati za dharula na kushirikiana na jamii ili kuimarisha lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru. Kila mwaka, WFP inawasaidia watu wapatao milioni 80 katika nchi 80.
 
Tufuatilie katika Twita: @wfp_tanzania; @wfp_media; @IrlEmbTanzania
 
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
 
Fizza Moloo, WFP, This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it., simu +255 (0) 784 720 022 au +255 (0) 692 274 729
Robert Hull, Ubalozi wa Ireland, This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it., simu  +255 22 260 23 55