Press Releases

Ubalozi wa Norway wachangia dola milioni 4.8 za Marekani kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania

TAARIFA YA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ubalozi wa Norway wachangia dola milioni 4.8 za Marekani kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania

Maeneo yatakayonufaika ni ya wakimbizi, wanawake na watoto

Oktoba 17 2016, Dar es Salaam– Ubalozi  wa Norway umeingia mkataba na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini, yakifanyakazi kama taasisi moja,  kuchangia dola za Marekani milioni 4.8 (sawa na shilingi bilioni 10.6) kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili. Mkataba huo ulitiwa saini kati ya balozi wa Norway nchini Tanzania, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez, katika ofisi za ubalozi wa nchi  hiyo jijini Dar es salaam.

Fedha hizo zimeelezwa kwamba zitaelekezwa kwenye shughuli zinazofanywa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kama kusaidia wakimbizi mkoani Kigoma, kuwawezesha wajasiriamali wanawake na kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo, Balozi wa Norway, Mheshimiwa Hanne-Marie Kaarstad aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwapa uraia wakimbizi wa Burundi 160,000, shughuli iliyofanyika Oktoba 2014.

Akitambua ongezeko jipya la wakimbizi kuanzia Mei 2015 katika mkoa wa Kigoma, alisema kwamba hali hiyo imeuweka mkoa huo katika mazingira magumu zaidi na hivyo zinahitajika juhudi za pamoja za kukabili hali hiyo.

Aidha alisema msaada kwa wakimbizi kupitia programu ya pamoja ya Kigoma, utawezesha kutekelezwa kwa mipango ya muda wa kati na mrefu ya kuwezesha mkoa kujitegemea kupitia shughuli mbalimbali za kuzalisha kipato.Alisema pia kwamba fedha hizo zitasaidia jamii inayoishi na wakimbizi hao.

Akizungumzia manufaa ya mfuko mmoja wa Umoja wa Mataifa wa hapa nchini, balozi Kaarstad  alisema kwamba yeye ni muumini mkubwa wa utendaji  kazi wa pamoja wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Ninaamini kama wengine wanavyoamini kwamba mfumo huo ndio mfumo bora unaowezesha Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake huku ikipunguza  gharama za uendeshaji. Ndio maana Norway imekuwa ikichangia Mfuko wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa. Mpaka sasa tumechangia dola za Marekani milioni 13.7 tangu uanzishwe na kwamba  tumeamua pia kuchangia pia UNDAP II kupitia mfuko huo”.

Pia alisema kwamba ofisi ya mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa inafanyakazi njema ya kuhakikisha kwamba mashirika ya Umoja wa Mataifa  nchini Tanzania yanawajibika ipasavyo kwa mujibu wa matarajio.

Balozi Kaarstad pia alielezea kuwa Norway itaendelea kuwa mtetezi wa haki za wanawake ; na kwa kuchangia UNDAP II wanaamini  watakuwa wametekeleza wajibu wao kwani wanawake kupitia ujasiriamali wataweza na hivyo kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema suala la kukomesha ukatili kwa wanawake linaenda sanjari na matamko ya Norway katika mapitio yake ya mwaka 2016 (UPR) yaliyopitishwa pia na serikali ya Tanzania.

Naye Bw. Rodriguez alishukuru serikali na wananchi wa Norway kwa mchango wao mkubwa katika kuwezesha Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake, huku akisema kwamba Norway imekuwa na mchango mkubwa katika programu mbalimbali za umoja huo nchini Tanzania.

 “Norway amekuwa mshirika mzuri wa Tanzania na Umoja wa Mataifa kwa miongo mingi wakiangalia mahitaji ya wale wasiokuwa na msaada, mchango wenu huu utasaidia kuangalia mahitaji ya walionyuma kabisa kama ilivyoelekezwa katika malengo endelevu ya dunia.”

Aidha Rodriguez alisema kwamba Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakifanyakazi kama taasisi moja yanataka kuimarisha uhusiano uliopo kati yao na Norway ili kusaidia Tanzania katika programu mbalimbali zitakazohakikisha kwamba wanawake na watoto wanahudumiwa kikamilifu.

Mchango wa Norway kupitia Mfuko wa Pamoja wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania utawezesha kutekelezwa kwa mpango wa msaada wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania kuanzia mwaka 2016-2021 (UNDAP II).

Msaada huo wa Norway utasaidia pia mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwawezesha wenyeji  wanaopokea wakimbizi kuwa na nafasi ya kufanya hivyo na hao wakimbizi pia kupata nafasi ya kuishi kibinadamu kwa kutatuliwa matatizo mbalimbali yanayowakabili.

Aidha fedha hizo zitachangia katika kuleta usawa na kukabili ukatili kwa wanawake na watoto.

 

Angalizo kwa Wahariri:

Norway na  mashirika ya Umoja wa Mataifa yakifanyakazi kama taasisi moja (One UN Tanzania) yamekuwa na uhusiano kwa muda mrefu wa kushirikiana na kwamba  hadi sasa Norway imechangia katika mfuko wa Mashirika hayo, zaidi ya dola za Marekani milioni 16 kusaidia mpango wa kwanza wa UNDAP (2011-2016).

Mchango wa sasa wa Norway utasaidia Umoja wa Mataifa katika mpango wake wa UNDAP II (2016-2021).

 

Kwa Maelezo zaidi tafadhali wasiliana na:

Victor Mlunde

Ofisa programu

Utawala na Masuala ya siasa

Ubalozi wa Norway, Dar Es Salaam

Simu ya mkononi: +255 782 777013/ +255 714 289428

Simu ya ofisi: +255 222 163 100

Tovuti: www.norway.go.tz

Facebook: https://www.facebook.com/Royal-Norwegian-Embassy-in-Dar-es-Salaam-946799618703270/

 

Hoyce Temu                                                                                       

Mtaalamu wa mawasiliano

Ofisi ya Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania

Simu ya mkononi: +255 682262627

Tovuti:    http://tz.one.org

Facebook: http://www.facebook.com/UNTanzania

Twitter:    @UnitedNationsTZ , @Alvaro_UNTZ