Press Releases

Umoja wa Mataifa wafikisha Malengo ya Dunia mkoani Simiyu

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI     

Imezuiwa hadi saa 06:30 mchana: Oktoba 13,2016

Umoja wa Mataifa wafikisha Malengo ya Dunia mkoani Simiyu

Vijana 400 kufikiwa na ujumbe wa maendeleo endelevu

Simiyu Oktoba 13, 2016: UMOJA wa Mataifa nchini Tanzania unaendelea na uelimishaji wa wananchi kuhusu malengo ya Dunia yaliyoelezwa katika Maendeleo Endelevu (SDGs), malengo ambayo sasa yana takribani mwaka mmoja.

Ili kuweza kufikisha malengo hayo kila mahali , Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na serikali utatumia wiki ya vijana kufundisha wanafunzi 400 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Simiyu ili wawe wakufunzi kwa wenzao.

Mafunzo hayo yamelenga kuwafanya vijana kuelewa na kuongeza ufahamu kuhusiana na malengo hayo ya dunia, hivyo kuwasaidia wenzao na wananchi wengine kutambua wajibu wao katika utekelezaji wake.

Mafunzo hayo mkoani Simiyu ni mwendelezo wa mafunzo yaliyozinduliwa mkoani Arusha na mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez.

Hadi sasa Umoja wa Mataifa umewezesha vijana 70 kutambua malengo hayo na kutumika kufunza wengine. Aidha wabunge zaidi ya 180 walipewa mafunzo hayo huku wahadhiri na wanafunzi 1,000 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa nao wamenolewa kuhusiana na malengo hayo ya maendeleo endelevu.

Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia umaskini, sera na uchambuzi, Bw. Mudith Cheyo alichangia katika mafunzo hayo kwa kueleza ni kwa namna gani serikali inatekeleza malengo hayo ya dunia. Bw. Cheyo amesema “Asilimia kubwa ya nguvukazi ya taifa letu ni vijana hivyo basi ni muhimu sana kuwashirikisha katika utekelezaji wa Malengo Ya Dunia katika ngazi ya taifa. Asilimia 34 ya nguvu kazi ni vijana, serikali imepanga mikakati kuhakikisha vijana wanapewa uwezo wa kuwawezesha kuzitumia fursa zilizopo kuleta maendeleo.”

Alisema kwamba kuwafunza vijana kuhusu malengo hayo ya maendeleo endelevu ni sehemu ya utendaji wa serikali katika utekelezaji wa malengo. Akizungumza katika semina ya malengo endelevu, Bw.Amon Manyama, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja huo(UNDP), alisema ajenda ya maendeleo kuelekea mwaka 2030 inahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu hasa vijana.

“Ni muhimu sana kwa vijana kuelewa Malengo Ya Dunia. Huu ni wakati wao. Kwa kuyaelewa malengo haya inrahisisha utekelezaji wake. Nimefurahi kuona muamko wa vijana waliojitekeza hapa leo na natumaini watawafikishia wengine ujumbe huu.” alisema na kuwapongeza vijana hao 400 kwa ushiriki wao katika kujifunza na kuelewa malengo hayo ya dunia na wajibu wa kila mmoja wetu.

Septemba 2015, viongozi 193 kutoka nchi mbalimbali duniani walikubaliana kuhusu malengo endelevu 17 kuelekea mwaka 2030.

Malengo hayo ambayo yanatakiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka 14 ijayo yanaleta kwa pamoja shughuli za kijamii, kiuchumi na kimazingira ili kuwa na maendeleo endelevu.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania yakifanya kazi chini ya mwavuli mmoja yanasaidia serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kwamba inafanikiwa katika kuyaingiza malengo yote 17 katika mpango wake wa maendeleo wa mwaka 2025 kupitia mpango wake wa kuisaidia Tanzania (UNDAP ll) ulioanza mwaka huu hadi mwaka 2021. Kwa bahati UNDAP II unaenda sanjari na mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021. (FYDP II).

 

Angalizo kwa Wahariri:

·Hadi kufikia mwakani inatarajiwa kwamba vijana 20,000 watakuwa wamefunzwa malengo ya milenia huku vijana 70 waliofunzwa maalumu wakiwafikia zaidi ya watu 6,000 tangu walipoanza uelimishaji Aprili mwaka huu.

·Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulifanya semina kwa wabunge 170 mkoani Dodoma katika masuala yanayohusiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Katika semina hiyo Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa aliwataka wabunge hao kuwa sauti, mabalozi na watathmini wa utekelezaji wa malengo hayo ya dunia katika majimbo yao.

 

Kwa mawasiliano:

Hoyce Temu                                                                                       

Mtaalamu wa mawasiliano

Ofisi ya Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa

Tanzania

 

Simu ya mkononi: +255 682262627

Tovuti: http://tz.one.org

Facebook: http://www.facebook.com/UNTanzania

Twitter: @UnitedNationsTZ , @Alvaro_UNTZ